KILA MTU NI MAHIRI KATIKA ENEO LAKE LA "KUJIDAI" NA REV. DR. ELIONA KIMARO

"Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake." - Warumi 8:28


Katika maisha unaweza usielewe maana ya jambo fulani wakati linapotokea ila baadae unaweza kuangalia nyuma na kushangaa namna jambo hilo lilivyokuwa la kipekee au namna linavyohusiana na mambo mengine. Yaani hata jambo ambalo unaweza kuliona ni baya, lenye kukupa tabu linaweza kuwa ni jambo lenye manufaa ila si rahisi kuona au kuelewa hivyo wakati linapotokea. Hivi ndivyo ilivyotokea kwangu mwaka 2019 nilipokutana na mtumishi wa Mungu Dr. Rev Eliona Kimaro kwa bahati "mbaya."



Ilikua siku ya Ijumaa miezi ya mwishoni mwa mwaka 2019 niliposhtuka kutoka katika usingizi mzito majira ya saa 11 alfajiri na kugundua nimepitiliza muda niliopanga kuamka. Usiku wa kuamkia siku hiyo nilikua nafanya kazi ya kuhariri kazi ya mteja ambayo ilifanyika mchana na ilitakiwa kukabidhiwa siku iliyofuata kwa ajili ya kutumiwa na vyombo vya habari hivyo ilinilazimu kuifanya kazi hiyo mpaka majira ya saa 8 usiku ili kuikamilisha. Kesho yake alfajiri nilikua na safari ya kuelekea Mwanza na baadaye Musoma kwa ajili ya kazi ya harusi siku iliyofuata lakini kwa sababu nilikua nimechoka sana nilijipumzisha kidogo wakati nangojea kukuche ila kwa kuwa nilikua nimechoka sana, sikuweza kuisikia alarm ilipoita. Niliwaza mpango wangu tayari ushaingia doa ila sikutambua kuwa unapopanga mipango yako na Mungu naye anapanga ya kwake na mipango yake haiepukiki.


Baada ya kukurupuka nikajiandaa haraka haraka na kumuita mara moja boda boda niliyekua nimemuandaa kunipeleka Airport. Tulitembea kwa mwendo wa haraka isio na kifani, tungeweza hata kupata ajali ila Mungu ni mwema tukafika salama. Njia nzima wazo langu na ombi langu kwa Mungu lilikua tu niweze kuwahi kwa sababu kuahirisha safari haikua option. Kwa bahati "mbaya" nilichelewa kwa dakika chache na tayari zoezi la checking-in lilikua limekwisha hivyo hawakuniruhusu kuingia. Nilijaribu kuwasihi na kuwaeleza namna safari yangu ilivyokua time-sensitive ila hawakuweza kunisaidia. Sikua na namna na niliona kama uzito wa dunia nzima umenielemea. Hakukua pia na nafasi katika ndege za mchana na muda huu tayari palishakucha na uwezekano wa kupata mabasi ya Mwanza pia haukuwepo, nisikia kukata tamaa nikamwomba Mungu anisaidie maana harusi sio kitu ambacho kinaweza kusubiri au kuahirishwa kutokana na kutokuwepo kwa mpiga picha. Punde si punde, muujiza ukatokea



Nilipata taarifa kuwa imepatikana nafasi moja tu katika ndege iendayo Kilimanjaro ila seat ni ya business class. Mtihani ni kwamba sikua na fedha ya kutosha kwa sababu kwenda Kilimanjaro ilimaanisha ingenilazimu kuzunguka KIA - Namanga - Nairobi - Sirari halafu Serengeti kwa sababu tayari jitihada za kutafuta usafiri wa Arusha - Serengeti zilikua zimegonga mwamba. Sikuwahi kupanda business class kabla ya siku ile na hata usafiri wa anga haukua kitu cha kawaida katika maisha yangu hivyo unaweza kuona namna tukio hili lilikua la kipekee. Nikajipa nguvu na kuamua kumueleza mteja wangu ule mkasa mzima na an imperfect solution iliyokua mbele yangu ambaye kwa bahati nzuri alinielewa na alikua tayari kuniongeza kiasi fulani cha fedha ili kufanikisha hiyo safari iliyonichukua karibu masaa ya 28 mfululizo mpaka kufika eneo la kazi. Nilifika majira ya adhuhuli wakati shughuli inakaribia kuanza hivyo ikanilazimu tena kuunganisha kufanya kazi mpaka usiku wa manane bila kupumzika. What a day to remember!


Nilipoingia katika ndege aina ya bombardier mali ya Shirika la ndege la Tanzania pembeni yangu alikua amekaa Mchungaji Dr. Kimaro. Sikuwahi kukutana naye kabla ya hii siku ila nilimfahamu tu kwa sura na reputation yake. Nakumbuka tulimsalimiana na baada tu ya ndege kuanza kupaa nilimuomba kama ninaweza kuzungumza naye mambo mawili matatu, alinikubalia bila kujiuliza mara mbili. Swali la kwanza na pekee nililomuuliza ni namna gani mtu anaweza kujua kusudi (purpose) la Mungu katika maisha yake? tuliendelea kuzungumza kwa kirefu mpaka tulipofika mwisho wa safari yetu na kabla ya kuagana nikamuomba kupiga naye picha akakubali. Sikuwahi kuiona tena wala kuifikiria tena ile moment mpaka leo hii miaka mitatu (3) baaadaye nilipokua napitia gallery yangu nikakutana nayo na kumbukumbu za mazungumzo yetu zikanijia. Nimepata msukumo wa kuandika makala hii ili wengine wapate kujifunza kupitia yale niliyojifunza kwake.

Kusudi la uumbaji (creation) wowote analijua muumbaji (creator). Hivyo kufahamu kusudi la kitu flani ni lazima uanzie na mtengenezaji/muumbaji. Kwa bahati nzuri Mungu tayari kupitia maandiko matakatifu ametueleza kusudi kuu la uumbaji wa mwanadamu ni kwa ajili ya utukufu wake (Isaya 43:7). Maana yake katika kipawa chochote kile alichokupatia, unapaswa kukitumia kuuendeleza ufalme wake na kumrudishia yeye utukufu. Haimaanishi kila kitu mtu afanye kazi kanisani au kuhudumu katika nyumba za ibada ila mahali popote ulipo na kwa chochote kile ambacho Mungu amekupa kufanya, utukufu/ukuu wa Mungu ukapate kuonekana. Biblia inatufundisha katika Mwanzo 1:26 kuwa binadamu wote tumeumbwa kwa mfano wa Mungu. Maana yake ndani yetu kila mmoja (sio tu watu baadhi) tuna sifa za kiungu na ndio maana watu waliotambua na kuliishi kusudi la Mungu katika maisha yao wana USHAWISHI mkubwa mahali popote walipo. Pia, ninaamini katika uumbaji kama asili ya binadamu wote na hivyo kufanikiwa kwetu kunapimwa na kama tumelitambua na kuliishi kusudi la uumbaji wetu. Swali kubwa ni namna gani basi unaweza kujua hilo kusudi (purpose) la Mungu katika maisha yako? Zipo ishara tatu (3) zinazoweza kukusaidia katika safari ya kutafuta kugundua kusudi la maisha yako na nimetumia neno safari kwa makusudi kwa sababu kwa hakika hii ni safari na kila mtu ana kituo chake, usafiri wa aina yake na ratiba ya safari anaijua Mungu mwenyewe. Eneo lako la "kujidai" ni pale ambapo hivi vitu 3 vinapokutana (intersect)...

1. TALANTA/ KIPAJI (TALENT)



Kila mtu ana kitu ambacho hata umshtukize usiku wa manane anaweza kukifanya bila mazoezi au maandalizi ya awali. Ila uwezo wa kukifanya vizuri zaidi (from good to great) utatokana na wewe kukifahamu hicho kitu, kuwekeza muda mwingi kukifanya, kuongeza maarifa zaidi juu ya hicho kitu na kwa kadri ya nguvu ambayo Mungu ameachilia nguvu ndani yako (Waefeso 3:20-21). Hiyo ndio tofauti ya watu wanaofanya vizuri (good) na wanaofanya vizuri sana (great).


2. UPENDO WENYE NGUVU (PASSION)


Waswahili wanasema pesa ni sabuni ya roho. Pesa ikiwepo watu wanaweza kufanya vitu visivyofikirika. Ila kama kipo kitu katika maisha yako ambacho unaweza ukakifanya VIZURI tena bila kutegemea malipo au recognition, safari yako inaweza kuanzia hapa. Wakati mwingine unaweza kukifanya hicho kitu kwa muda mrefu bila kuchoka au usigundue ni muda kiasi gani umepita mpaka unaposhtuka kuaangalia saa na bado roho yako ikawa na furaha, basi inaweza kuwa ishara kwamba unafanya kitu sambamba na kusudi la Mungu katika maisha yako. Ukikifahamu hicho kitu na kukizingatia, possibilities are endless (Mhubiri 9:10, Mithali 22:29). Muombe Roho Mtakatifu akusaidie kukitambua maana viko vingi ving'aavyo lakini si vyote ni dhahabu.


3. FURSA (OPPORTUNITY)


Mungu anapokua ameweka jambo ndani yako lazima atakupa na fursa ya kulifanya/kulitendea kazi. Kwa uzoefu, mara nyingi hizi fursa huwa zinakuja kwa namna ambayo wewe mwenyewe unaweza kushindwa kuzielewa. Fursa hizi hujivika sura ya matatizo/changamoto zinazohitaji ufumbuzi na wewe ndio mtu unayeweza kuzitatua. Inahitaji ujasiri, uthubutu na Neema ya Mungu kuweza kuzitambua hizi fursa na kuzichangamkia. Kila tatizo/changamoto unayotatua inakusogeza karibu zaidi na kusudi la Mungu kwenye maisha yako. Hivyo basi ukikutana na changamoto usizikwepe hata kama unafikiri hauna uwezo wa kuzitatua. Unapaswa kujiamini na kuamini kuwa Mungu hawezi kukupa mtihani usioweza kuufaulu (1 Wakorinto 10:13). Ukishindwa kujiamini, mwamini Mungu.



Kwa kuhitimisha, nakushauri ukitafute na kukisoma kitabu alichokiandika Mchungaji Dr. Kimaro kiitwacho "KUTOKA NDOTO HADI HATIMA". Kama wewe una ndoto, maono au bado haujajua kusudi la Mungu katika maisha yako na unatamani kupata maarifa zaidi kutoka kwa mtaalamu wa mambo ya kiroho basi hiki kitabu ni kwa ajili yako. Kimebadilisha maisha na mtazamo wangu juu ya mambo mengi na ni imani yangu pia kwamba kinaweza kubadilisha ya kwako. Mungu akubariki!

Geofrey Mtatiro

I'm a storyteller by trade but a problem-solver by birth. I find creative ways to tell stories of Individuals, Brands, Businesses & Organizations through Photography, Film Production & Advertising. In 2012, I founded BRAINBONGO to do just that while still in high school with the help of a few friends. Through the years, we have become really good at it. We love it and we live it. We are #EXTRAORDINARY!

Post a Comment

If you like this post be sure to leave a comment and share it with your friends. It will make my day!

Previous Post Next Post

Contact Form